Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemwonya na kumwambia Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), kwamba kadi za onyo kwa ajili yake zimeisha kutokana na kushindwa kuhudhuria mahakamani siku ya kesi.
Kauli hiyo ilitolewa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi baada ya kubaini kwamba ilitolewa hati ya kumkamata mbunge huyo kwa kushindwa kufika mahakamani.
Halima Mdee alipotakiwa kujitetea aliinuka na kujieleza kuwa amefika mahakamani hapo akiwa na nyaraka za safari ikiwamo tiketi na VISA na kwamba taarifa za safari alimpa wakili.
Kwa upande wa wakili wao, Hekima Mwesiga aliieleza mahakama kuwa nyaraka za kuiarifu mahakama juu ya safari ya Halima Mdee nje ya nchi kwa bahati mbaya hakuziwasilisha, alikuwa nazo Peter Kibatala ambaye alikuwa akiendesha kesi ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Mdee na wabunge wengine wa Chadema, Mwita Waitara, Saed Kubenea na makada wao wanatuhumiwa kumjeruhi Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Theresa Mmbando.