Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali maombi yaliyowasilishwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ya kutaka asikamatwe hadi kesi yake ya kikatiba dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda itakapomalizika.
Maombi hayo yalitupwa kwa sababu kifungu cha sheria kilichotumika kuyafungua si sahihi na kwamba hutumika pale ambapo sheria ziko kimya.
Uamuzi huo wa majaji umefikiwa kutokana na pingamizi la jamhuri lililowasilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu Gabriel Malata kuiomba kuyatupilia mbali maombi hayo kwani hayana msingi kisheria.
Katika hatua nyingine, mwanahabari nguli nchini Jenerali Ulimwengu, ameungana na jopo la mawakili Tundu Lissu, Peter Kibatala na John Malya katika kumtetea Mbowe.
Mbowe amefungua kesi hiyo ya kikatiba namba 1, ya mwaka 2017 dhidi ya wadaiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam. Kesi hiyo itasikilizwa tena Machi 8, mwaka huu.