Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam imefuta maombi ya kesi ya kikatiba iliyofunguliwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe.

Kutupwa kwa kesi hiyo kumetokana na mahakama hiyo kukubali pingamizi la walalamikiwa kwamba mahakama hiyo haina mamkala ya kuyasikiliza.

Walalamikiwa katika maombi hayo ni  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamishna wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Siro na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam (ZCO), Camillius Wambura.

Uamuzi huo ulitolewa jana na jopo  la majaji watatu, likiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji Sekiet Kihiyo, akisaidiana na Pellagia Khaday na Dk. Lugano Mwandambo.

Akisoma uamuzi huo kwa niaba ya jopo, Jaji Khaday alisema upande wa walalamikiwa uliwasilisha pingamizi la awali kwamba mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza maombi hayo kwa sababu mlalamikaji alitakiwa kuwasilisha katika mamlaka husika.

Pia sheria za haki za msingi kifungu cha 8 kidogo cha (2) sura ya 3, inakataza mahakama hiyo kusikiliza maombi kama hayo na kwamba kuna mamlaka zinazoshughulikia kabla ya kufikishwa mahakamani kwa sababu si kesi ya kikatiba.

Aidha, mahakama imetoa uamuzi huo baada ya mlalamikaji kushindwa kufika mahakamani kuwasilisha majibu ya pingamizi la awali la walalamikiwa hata baada ya kupewa muda wa kufanya hivyo.

Katika kesi ya Msingi ya Kikatiba Mbowe alikuwa anapinga kitendo cha polisi kumtaka afike kituoni kwa madai kuwa ni utekelezaji wa amri ya Mkuu wa Mkoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *