Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa Tanzania itaendeleza uhusiano na ushirikiano wake mzuri na nchi jirani ya Msumbiji licha watanzania kuondolewa nchini humo.

Rais Magufuli ametaka suala la wahamiaji haramu wanaoondolewa nchini humo wakiwemo Watanzania lisikuzwe huku akisisitiza kuwa Serikali haiwezi kuwatetea watu wanaoishi katika nchi nyingine bila kufuata sheria.

Kauli hiyo ameitoa jana kwenye mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mashujaa Mjini Mtwara kabla ya kuhitimisha ziara yake ya siku 4 katika mikoa ya kusini ambapo amemaliza jana na kurejea Dar es Salaam.

Katika mkutano huo Rais Magufuli amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuhakikisha inasukuma maendeleo ya Mtwara na Lindi kwa nguvu kubwa kwa manufaa ya wananchi.

Pia amesema kuwa Serikali imedhamiria kutilia mkazo juhudi za uendelezaji wa bandari ya Mtwara, ujenzi wa barabara, uimarishaji wa miundombinu ya nishati ya umeme, ujenzi wa viwanda vikubwa na usimamizi mzuri wa shughuli za kilimo ambavyo vitasaidia kukuza uchumi, kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya watu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *