Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli amempongeza Balozi Prof. Joram Biswaro kwa kuteuliwa kuwa Mwakilishi Maalum wa Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika na Mkuu wa Ofisi ya Umoja huo Sudan Kusini.
Prof. Biswaro ameteuliwa na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) Dk. Nkosazana Dlamini-Zuma na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Brigedia Jenerali Sara Thomas Rwambali ambaye amemaliza muda wake.
Katika pongezi hizo Rais Magufuli amesema Tanzania imepokea uteuzi huo kwa heshima kubwa na ipo tayari kutoa ushirikiano atakaohitaji Balozi Biswaro katika utekelezaji wa majukumu yake.
Dkt. Magufuli amemtakia heri Prof. Biswaro katika majukumu hayo mapya na amemshukuru na kumpongeza Brigedia Jenerali Sara Thomas Rwambali aliyemaliza muda wake kwa uwakilishi mzuri katika kipindi chake.
Rais Magufuli ambaye ndiye aliyempendekeza Balozi Biswaro kushika nafasi hiyo, amemshukuru Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika Dk. Nkosazana Dlamini-Zuma kwa kuridhia mapendekezo yake.