Serikali imeyafungia maghala matano ya kuuza vinywaji vya jumla kutokana na kukosa vibali vya kuruhusu kufanyika kwa biashara hiyo.

Maghala hayo yamefungwa katika operesheni maalumu inayoendelea ya utekelezaji wa maelekezo ya serikali ya kusitisha uzalishaji, usambazaji, uingizaji, uuzaji na matumizi ya pombe kali zilizofungashwa kwenye vifungashio vya plastiki (viroba).

Kiongozi wa operesheni hiyo wilaya ya Kinondoni ambaye ni Mkaguzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), John Nzila alisema maduka hayo yakiwemo yale yaliyokamatwa na mzigo juzi, hayakuwa na vibali.

Alisema ili mtu aweze kufanya biashara kama hizo za vinywaji, ni lazima awe na cheti cha TFDA na TBS, cheti cha Tathmini ya Athari ya Mazingira (EIA) na awe analipa kodi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA). Alisema maduka hayo yakiwemo yale yaliyokamatwa na viroba juzi, yamefungiwa hadi taratibu zitakapokamilika.

Kwamba bidhaa zilizokutwa, wamezidhibiti hadi utaratibu mwingine wa serikali utakapotangazwa.

Kwa upande wake, msimamizi wa operesheni hiyo wilaya ya Mkuranga, Aron Nzalla ambaye ni Mkaguzi wa TFDA, alisema wameyafungia maghala ya Bonju General Enterprises lililopo Mkuranga na Mama Mkwe lililopo Vikindu kutokana na kukosa vibali vyote pamoja na kubainika kuuza viroba juzi.

Alisema operesheni hiyo imeonesha mafanikio kwa baadhi ya maduka, ambapo tayari wafanyabiasahara wengi wametii agizo la serikali na kuacha kuuza pombe kali za viroba.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *