Zaidi ya magari 200 yaliyokuwa yanatumiwa na rais nchini Ghana yamepotea na hayajulikani yalipo baada ya serikali mpya kuingia madarakani.
Chama tawala kilihesabu magari hayo mwezi mmoja kabla ya kuingia madarakani baada ya kupata ushindi uchaguzi wa mwezi Desemba mwaka jana.
Imekuwa kawaida kwa baadhi ya maafisa wa serikali inayoondoka kutorejesha magari ya serikali, na hulazimu serikali mpya kuyatwaa kwa nguvu nchini Ghama.
Waziri mmoja katika serikali iliyoondoka ya John Mahama hata hivyo amesema kuenezwa kwa habari kwamba wenzake walitekeleza uhalifu ni makosa.
Msemaji wa rais Eugene Arhin aliambia wanahabari kwamba maafisa wa serikali mpya walipata magari:
- 74 kati ya196 aina ya Toyota Land Cruiser
- 20 kati ya 73 aina ya Toyota Land Cruiser Prado
- 11 kati ya 24 aina ya Mercedes
- mawili kati ya 28 aina ya Toyota Avalon
- mawili kati ya sita aina ya BMW.
Kituo cha redio cha Citi FM nchini Ghana kimeripoti kwamba rais amelazimika kutumia gari aina ya BMW lililoundwa miaka 10 iliyopita kutokana na kutorejeshwa kwa magari hayo.