Muandaaji wa Shindano la Bongo Star Search (BSS), Madam Ritha ameomba radhi mbele ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Harrison Mwakyembe kwa kuchelewesha malipo ya Mshindi wa BSS mwaka 2019, Meshaki Fukuta.
Madam Ritha ameyasema hayo jana katika uzinduzi uliofanyika kwenye Hoteli ya Slipway iliyopo Msasani, Dar na kuhudhuriwa na wadau kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Basata, Bodi ya Filamu wengineo.
Madam Rita aliomba radhi kufuatia changamoto ya utoaji wa zawadi ya mshindi wa kwanza katika shindano lililopita Meshack Fukuta.
Madam Rita akiendelea kuomba radhi alisema hayo yalisababishwa na wadhamini aliowaamini jambo ambalo kwa upande wake hakutegemea kama lingeweza kumuweka katika picha mbaya katika jamii.
Baada ya kusema hayo Madam Rita alimkaribisha Waziri Mwakyembe kwa ajili ya uzinduzi huo ambapo alimpongeza Madam Rita kwa kuomba radhi na kusema huo ndiyo uungwana na kumuonya kumtaka kuwa makini ili mambo kama hayo yasiweze kujirudia tena.
Msimu wa mwaka huu unatarajiwa kuanza kusaka vipaji Septemba 19 mkoani Mbeya, Arusha Septemba 26, Mwanza Oktoba 3, Dodoma Oktoba 10 na Dar es Salaam itakuwa Oktoba 17 na 18 mwaka huu.