Chama cha Madaktari nchini Tanzania (MAT) kimepinga mpango wa Serikali kutuma madaktari 500 nchini Kenya kutokana na upungufu wa madaktari uliopo hapa nchini.

Pingamizi hilo linafuatia makubaliano kati ya serikali ya Tanzania na Kenya mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo Tanzania ilikubali kutuma madaktari wapatao 500 nchini Kenya.

Maafisa wa chama cha MAT wamesema, wanahitaji ufafanuzi kuhusu ni kwa nini Serikali ya Kenya imeshindwa kuajiri Madaktari wake na kuanza kutafuta Madaktari kutoka Tanzania huku ikizingatiwa kwamba malipo ya Madaktari wa Tanzania yatakuwa makubwa zaidi ya wenyeji.

Kadhalika taarifa iliyotolewa na MAT imehoji ni kwa nini suala hili linafanyika wakati Kenya ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu, na kuhoji pia nani atawajibika katika suala la usalama wa Watanzania hasa ikizingatiwa kwamba tayari kuna viashiria vya chuki, na ikizingatia Kenya bado ina changamoto za kiusalama.

MAT imesisitiza kwamba ni muhimu kusitisha zoezi la kuwapeleka Madaktari wa Tanzania mpaka hapo Serikali ya Kenya itakapoanza utekelezaji wa makubaliano kati yake na Madaktari wao,

Kenya imeshuhudia mgomo wa madaktari uliomalizika wiki iliyopita baada ya kudumu kwa siku 100.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *