Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amemwandikia barua Gavana wa Benki ya Tanzania (BoT), Profesa Beno Ndulu ili achukue hatua za kulishughulikia sakata la fedha za ruzuku zinazodaiwa kukwapuliwa na CUF upande wa Mwenyekiti anaetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.
Maalim Seif ameandika barua yenye kumbukumbu namba CUF/HQ/AKM/003/017/01 na nakala zingine kuzituma kwa mamlaka mbalimbali.
Katika barua hiyo kwa Profesa Ndulu, Maalim ameambatanisha kumbukumbu ya miamala ya fedha ilivyofanyika, pia amesema kuwa chama hicho kinaendelea na taratibu za kukamilisha hatua za kisheria ili kuwafikisha mahakamani wahusika wote walioshiriki katika kuchukua fedha hizo, akiwapo Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi.
Amesema kuwa, Mutungi atakuwa na kesi ya pili na atashtakiwa kutokana na madai ya kushirikiana na walalamikiwa wale wale wa kufungua akaunti mpya ili wapewe ruzuku.
Aidha, amesema Jaji Mutungi amefanya hivyo huku akifahamu fika kuwa kuna kesi ya msingi iliyopangwa kusikilizwa Februari 2, 2017 mbele ya Jaji Kihiyo.
Hata hivyo, hivi karibuni CUF upande wa Maalim Seif ulilalamikia hatua iliyochukuliwa na Jaji Mutungi kuwapa CUF upande wa Profesa Lipumba zaidi ya shilingi milioni 360 za ruzuku.