Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ameeleza maendeleo ya afya ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), baada ya kumtembelea hospitalini Nairobi, Kenya.
Maalim Seif amesema kuwa Lissu anaendelea vizuri na hajapoteza mwelekeo kutokana na tukio hilo.
“Bado hajapoteza mwelekeo akili yake ipo timamu, ametuhakikishia haya yaliyotokea hayatamrudisha nyuma katika kuwatetea wanyonge.
“Anazungumza vizuri, yuko makini sana anajua anachokisema na mimi nimepata moyo jinsi nilivyomuona,” alisema Maalim Seif.
Alisema kutokana na mambo yanayoendelea nchini, lazima kuwapo na mjadala wa taifa kuona tumekosea wapi na kujirekebisha.
“Mambo kama haya kutokea Tanzania ni jambo ambalo kila Mtanzania lazima aingiwe na wasiwasi kwa sababu hakuna hata mmoja na hasa mwanasiasa ambaye ana usalama wa maisha yake.
Kuhusu uchunguzi wa tukio hilo, alisema hata kama vyombo vya dola vya ndani vitafanya si aibu kwa nchi kutafuta msaada kwa wengine.
Lissu alipigwa risasi zinazokadiriwa kufikia 32, Septemba 7, mwaka huu, alipokuwa akirejea nyumbani kwake Area D mjini Dodoma baada ya kutoka kuhudhuria kikao cha Bunge na kujeruhiwa vibaya sehemu mbalimbali za mwili wake.