Wizara ya Ardhi, Maji, Nishati na Mazingira ya Zanzibar imesema imedhamiria kuimarisha maabara za Mamlaka ya Majisafi na Salama Zanzibar (ZAWA) kwa ajili ya kutoa huduma kwa kuzingatia ubora unaokwenda sambamba na ushindani wa kibiashara.
Hayo yalisema na Waziri wa wizara hiyo, Salama Aboud Talib wakati akijibu swali lililoulizwa na Mwakilishi wa Jimbo la Paje, Jaku Hashim Ayoub aliyetaka kujua mikakati ya kuimarisha maabara za Zawa ili kwenda sambamba na ushindani wa biashara na kuimarisha afya za wananchi na kuepukana na maradhi ya mlipuko ikiwemo kipindupindu.
Talib alisema hivi sasa taasisi ya Zawa inafanya kazi zake kwa misingi ya kibiashara na huduma kwa wananchi katika kulinda afya zao kwa hivyo suala la kuimarisha maabara ni muhimu.
Kwa mfano, alisema kuanzia sasa maji yote yanayosambazwa na mamlaka ya maji safi na salama kwenda kwa wananchi yanawekwa dawa ya chlorine ya kupambana na kudhibiti maradhi ya mlipuko.