Mwezi April mwaka huu mwimbaji, Lulu Diva aliachia wimbo wake “MAMA” ambao ulishika hisia za wengi kwani alizungumza kuhusu hali ya maradhi ambayo anaipitia Mama yake mzazi.
Diva ametueleza kwa kina chanzo cha maradhi ya mama yake ambapo kauli kubwa iliyogusa hisia kwenye mahojiano haya ni kwamba Mama yake hajazungumza kwa miaka 9 sasa.
Tukio hilo ambalo limekuwa pigo kuu katika maisha yake, lilianza miaka tisa iliyopita wakati mama yake mzazi alipoanza kuumwa ugonjwa ambao ulimuathiri kiakili. Tangu wakati huo hadi leo Lulu anasema mama yake mzazi hajazungumza wala kutembea mwenyewe.
Kilio kikuu cha msanii huyu ni kuwa wakati anaanza kupata kipato cha kumuwezesha yeye na mama kuishi maisha ya stara kuliko maisha ya taabu walikotoka, ndio wakati mama yake alianza kuumwa ugonjwa ambao umekuwa ukiwasumbua kwa muda mrefu.
“Mama hajazungumza kwa miaka tisa, sijui anafikiria nini?, sijui ananiwazia yepi na hata sielewi yuko katika dunia ipi? Ni jambo linalonikosesha usingizi. Najiuliza na usanii huu wangu mama hajaweza kunishabikia kwani haelewi kinachofanyika, inauma sana kumuona mama akiwa katika hali hii.” alieleza Lulu Diva.
Kwa miaka tisa hii, Lulu hajaweza kuzungumza na mama yake, na hata akimzungumzisha kutokana na maradhi yake hana uwezo wa kujibu, na Lulu hajui kama anatambua ama hatambui akizungumzishwa.
Hilo linamtatiza sana Lulu, anasema anajivunia mwaka 2018 kupitia kipato chake cha muziki aliweza kumpeleka mama yake hospitalini alikofanyiwa upasuaji sehemu ya kiuno, lakini baada ya kuruhusiwa kutoka hospitalini, mama alipata ajali na akavunjika mguu.