Mwanamuziki wa Bongo Fleva, Lulu Diva amewashukuru wote waliomshika mkono kipindi mama’ke mzazi alipofariki dunia.
Lulu Diva ametoa shukrani zake za dhati kwa mashabiki wake na Serikali kwa mchango waliotoa wakati ambapo alikuwa anapitia kipindi kigumu kwa kumpoteza mtu ambaye alikuwa msingi wa maisha yake.
“Hii ni kwa kila mmoja aliyejitoa juu yangu kwa hali na mali, wasanii wenzangu, viongozi mbalimbali, vyombo vya habari, wadau tofauti, mashabiki zangu, ndugu, jamaa marafiki na watanzania wote walioguswa kwa ujumla, iwe kwa kuja kuniona, kwa kunipigia simu, kwa kusafiri na mimi, kwa posti za faraja na kwa namna yoyote ile, kutoka moyoni mwangu kabisa nawashukuru sana sana wote na ninathamini,” anasema Lulu Diva.
Lulu Diva amekiri kwamba mapenzi yake kwa mama’ke yalikuwa mazito hivyo itamchukua muda mrefu kukubali kwamba hatamuona tena kipenzi chake.
Lulu Diva pia hajakosa kushukuru kampuni zote anazoshirikiana nazo kibiashara kwa kusimama naye kidete mpaka wakati mipangilio ya safari ya mwisho ya mamake ilipokamilika.
Kwa mujibu wake, amekuwa akijifungia ndani tangu kuondokewa na mzazi wake huyo kutokana na uzito wa tukio hilo ila amesema kwamba ameamua kukubali hali kwa kuwa Mungu ndiye hutoa na ndiye hutwaa.