Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameagiza wananchi wote wanaomiliki viwanja vya makazi kuhakikisha wanachukua hati za umiliki ifikapo Machi 30, mwakani.
Pia amemuagiza mwekezaji wa mgodi eneo la Maganzo wilayani hapa kuwalipa fidia wananchi wanaomiliki mashamba na wenye nyumba walipwe fidia zinazofanana na thamani ya nyumba zao.
Ametoa maagizo hayo mwishoni mwa wiki wakati alipofanya ziara wilayani Kishapu, Mkoa wa Shinyanga, ambako alisikiliza na kutatua kero za wananchi kuhusu sekta hiyo.
Lukuvi amesema serikali imedhamiria kutatua kero za ardhi na ina mkakati wa kuwasaidia wananchi wawe na hati halali za viwanja wanavyomiliki huku akiwaahidi kupata hati zao ndani ya mwezi mmoja kwa atakayelipia mapema.
Akizungumza na wananchi mjini Mhunze, Lukuvi alisema suala la hati ni la lazima na kuwa inamsaidia mwananchi kuwa na usalama na kiwanja chake na kupata huduma mbalimbali kama mikopo ya benki.