Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amemtahadharisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, John Wanga endapo atashindwa kusimamia vema agizo la urasimishaji makazi holela na uandaaji wa hati miliki kwa wananchi atatumbuliwa.
Alitoa tahadhari hiyo juzi baada ya kusomewa taarifa ya utekelezaji wa urasimishaji na uandaaji wa hati za ardhi ambako Halmashauri ya Ilemela imetekeleza kwa asilimia moja kwa kuandaa hati 834 huku viwanja vingine 16,000 vikiwa vimepimwa bila kuandaliwa hati.
Lukuvi ambaye alionekana kukasirishwa na hali hiyo alisema kushindwa kuandaliwa hati hizo ndani ya Halmashauri ya Ilemela ambayo ina maofisa ardhi na watathmini zaidi ya 40 kmeisababishia hasara Serikali.
Alisema kazi hiyo ingefanyika ilivyotarajiwa serikali ingepata mapato ya Sh bilioni 2.5 kwa mwaka lakini kilichopatikana ni Sh bilioni 1.3 tu.
Waziri alisema Halmashauri za Ilemela na Nyamagana zinatakiwa zikamilishe hatua hiyo Juni 30, mwaka huu atakapoifunga rasmi na kutangaza ‘masterplan’ ya Jiji la Mwanza ifikapo Agosti.
Aliwataka wananchi kutambua kuwa baada ya kufungwa urasimishaji makazi haitatokea tena fursa ya namna hiyo.
Amesema wananchi ambao hawatakuwa na hati ya eneo analoishi watahesabika kama wavamizi, hivyo watapoteza haki yao na maeneo hayo yatachukuliwa na Serikali kwa shughuli nyingine.
Lukuvi amesema Serikali kuu imetenga Sh bilioni 22 kwa ajili ya masterplan ya Mwanza ambayo itaanza kutekelezwa Agosti mwaka huu, kazi ambayo itafanywa na wataalamu kutoka China.
Source: Mtanzania