Mjumbe wa kamati kuu ya (CHADEMA), Edward Lowassa amefunguka na kutoa pole kwa aliyekuwa Rais mteule wa Kenya Uhuru Kenyatta kufutia mahakama ya juu nchini humo kufuta matokeo ya uchaguzi wa Urais uliofanyika Agosti 8, 2017.

Lowassa anasema yeye bado ataendelea kumuunga mkono Uhuru Kenyatta kwani ni kiongozi mwenye kusimamia Demokrasia na mwenye maono ambaye anaweza kuisadia Kenya hivyo ataendelea kumuunga mkono tena katika uchaguzi utaofanyika upya nchini humo.

Lowassa amesema kuwa “Nitumie nafasi hii kumpa pole Uhuru Kenyatta kwa jambo lililotokea lakini nimpongeze kwa kufanya kampeni ya kiume kafanya kazi nzuri sana, ukitazama maoni ya waangalizi mbalimbali walisema uchaguzi ulikuwa wa huru na haki, lakini pia ukitazama orodha ya washindi wa wabunge Jubilee ndiye inaongoza, kwa maseneta na magavana Jubilee ndiyo inaongoza picha hizi mbili zinatoa picha, lakini ikishasema mahakama maamuzi yake ni lazima yaheshimike”.

Lowassa amesema kuwa anamuheshimu sana Uhuru Kenyatta kutokana na jinsi ambavyo anaheshimu Demokrasia na kudai katika kipindi cha uongozi chake siku zote amekuwa akilinda Demokrasia ya nchi hiyo kwani wabunge wamekuwa na haki na vyama vimekuwa na haki na kila mtu ana haki.

Pia amesema kuwa “Niliwahi kumsikia mama mmoja akimtukana Uhuru Kenyatta matusi ya nguoni kabisaa kiasi kwamba yule mama angekuwa hapa Tanzania siku nyingi angekuwa jela lakini Uhuru Kenyatta alimsamehe na maisha yakaendelea lakini uongozi wake ni uongozi wenye malengo amerithi nchi iliyotoka kwenye ugomvi wa kivita lakini ameweza kuingoza kwa miaka mitano kimya wakifanya maendeleo, na kwa maendeleo nadhani wametupita kwa sababu Uhuru Kenyatta kwa hiyo ni mtu mwenye upeo, makini na mahiri ambaye anaitakia mema Afrika na Afrika Mashariki”.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *