Shirikisho la soka nchini ‘TFF’ limetoa ratiba rasmi ya Ligi kuu Tanzania Bara msimu wa 2016/2017 ambapo ligi hiyo inatarajiwa kuanza Agosti 20 mwaka huu.
Mabingwa watetezi, Yanga SC wataanza kwa kucheza dhidi ya JKT Ruvu Agosti 31 Uwanja wa Taifa, Simba wataanza kumenyana dhidi ya Ndanda katika uwanja wa Taifa Agosti 20 na Azam FC wataanza kwa kucheza dhidi ya African Lyon katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamanzi jijini Dar es Salaam.
Mechi nyingine za ufunguzi wa ligi hiyo zitakuwa kama ifuatavyo, Kagera Sugar atacheza na Mbeya City Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting Uwanja wa Manungu, Morogoro, Majimaji na Prisons Uwanja wa Majimaji, Songea, Stand United dhidi ya Mbao FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Toto Africans na Mwadui FC Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwaza.
Yanga SC ambaye ni bingwa wa ligi hiyo atamenyana na Azam FC ambaye ni mshindi wa pili wa ligi kwenye mechi ya Ngao ya Jamii itakayofanyika katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Agosti 17 mwaka huu.