Mbunge wa zamani wa Jimbo la Kahama, James Lembeli amemtaka Rais, Dk. John Magufuli kuhakikisha anakisafisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Lembeli ambaye mwaka jana alijiengua ndani ya CCM na kujiunga na Chadema, alisema ikiwa Rais Magufuli atafanya hivyo, yuko tayari kurejea CCM.
Mwanasiasa huyo aliondoka CCM kwa kile alichodai kuwa chama hicho kimekithiri vitendo vya rushwa pamoja na unafiki miongoni mwa wanachama na viongozi wake.
Lembeli alizungumza jana mjini Kahama baada ya kuitwa kuwasalimia wananchi katika mkutano wa Rais pia alimshukuru Rais Magufuli kufika wilayani Kahama, ambapo alisema hana kinyongo na kwamba ataendelea kusalimiana na watu mbalimbali, kwani kubadili msikiti si mwisho wa uislamu.
Akizungumza na wananchi wa Mji wa Kahama, Rais Dk. Mgufuli, amesema yote aliyoyaahidi atayafanyia kazi na kuongeza kuwa hatalewa madaraka ya urais na kuwataka Watanzania kumtanguliza Mungu katika kazi wanazozifanya za kila siku.
Pamoja na hali hiyo Rais Magufuli, alimtaka Lembeli, kurejea ndani ya CCM kwani chama alichokuwa nacho kwa sasa ndipo walipo mafisadi aliokuwa akiwazungumzia kila siku.
Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM taifa, amesema katika kuonesha dhamira ya kupambana na ufisadi, tayari Serikali yake imetenga Sh bilioni 2.5 kwa ajili ya kuwashughulikia mafisadi.