Leo ni kumbukumbu ya miaka 45 tangu Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume kuuawa kwa kupigwa risasi katika jengo la Makao Makuu ya Chama cha Afro-Shirazi (ASP) visiwani mjini Zanzibar mnamo tarehe 7 Aprili, 1972.
Mara tu baada ya mauaji hayo kufanyika hali ya hatari ilitangazwa nchi nzima ikifuatana na msako mkali uliohusisha watu kadhaa kutoka katika vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na raia huku taarifa zikimtaja Abdulrahman Muhammed Babu kuwa muhusika mkuu
Hadi leo hii hakuna ukweli thabiti juu ya kifo cha Hayati Karume maana wengine wanahusisha kifo chake na chuki za siasa na mengineyo.
Japokuwa Mjane wa Karume (Bi. Fatma Karume) anasema hakuwa akifahamu kifo cha Mzee Karume mpaka alipokuja kuambiwa na mdogo wake kuwa ameona gari ya mzee imetoka bila ya kuwa na mtu ndipo alipojaribu kumpigia Kamishna wa Polisi enzi hizo Mzee Kisasi lakini hakufanikiwa kumpata kwa kuwa naye alikuwa ameshaenda hospitalini alipokuwa amehifadhiwa baada ya kupigwa risasi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na mjane wa Rais wa kwanza wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mama Fatma Karume wakati alipomtembelea nyumbani kwake
Aidha Bi. Fatma amesema alipofika katika hospitali ya Muungano alizuiliwa kuingia ndani na wanajashi waliokuwa wametanda eneo hilo kwa bahati nzuri mwanaye Haji Mrisho naye alikuwa ni miongoni mwa wale wanajeshi akapata wepesi wa kuingia na kumuona Karume akiwa amelazwa chini ameshafunikwa shuka.
Pamoja na hayo amesema siku ya maziko aliweza kuonana Mwalimu Nyerere wakakumbatiana lakini hakuweza kujua kilichoendelea hapo kwa kuwa alipoteza fahamu kutokana na majonzi aliyokuwa nayo.
Kwa vyovyote vile, jina la Abeid Karume haliwezi kusahaulika katika historia ya ukombozi wa visiwani humo kutokana na misingi aliyowajengea Wazanzibar.