Korea Kaskazini imeionya Marekani kutoanzisha vitendo vya uchokozi katika eneo la Korea ikisema kuwa iko tayari kulipiza kisasi kupitia mshambulio ya kinyuklia.
Taifa hilo limesema hivyo wakati ambapo kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un, amehudhuria gwaride la heshima katika mji mkuu wa Pyong yang, akiadhimisha siku ya kuzaliwa ya babu yake, marehemu Kim II-Sung, ambaye ni mwanzilishi wa taifa hilo.
Huku kukiwa na wasiwasi kwamba Korea Kaskazini inakaribia kupata ufanisi wa kukamilisha silaha za Kinyuklia, Gwaride la Jumamosi ilikuwa fursa kwa bwana Kim kuonyesha uwezo wa kijeshi wa taifa hilo.
Vifaa vilivyoonyeshwa kwa mara ya kwanza vilikuwa vile vilivyotajwa kuwa manuwari za Pukkuksong ,makombora ya masafa marefu yanayoweza kwenda kwa takriban kilomita 1000.
Wachanganuzi wa vifaa vya kijeshi pia wanasema kuwa kuna makombora mawili mapya yanayoweza kurushwa kutoka bara moja hadi jingine, lakini haijulikani iwapo yamefanyiwa majaribio.
Kulikuwepo na sherehe za kawaida, kama vile mamia ya wanajeshi kupiga gwaride na msafara wa magari ya kivita huku yakiwa yamebeba silaha kama vile makombora.