Kiongozi mkuu wa upinzani nchini Zimbabwe Morgan Tsvangirai amefariki dunia nchini Afrika kusini.
Kwa mujibu wa kiongozi Mwandamizi wa chama cha MDC, Tsvangirai mwenye umri wa 65, na aliyewahi kushika nafasi ya Uwaziri mkuu nchini Zimbabwe ameripotiwa kuwa alikuwa akisumbuliwa na Saratani ya utumbo.
Makamu Rais wa chama chama cha MDC Elias Mudzuri ameliambia Shirika la Habari la Uingereza Reuters kwamba marehemu alifariki jioni ya Februar 14.
Katika kipindi cha uhai wake, maisha yake ya kazi yaligubikwa na harakati nyingi za kisiasa dhidi ya mpinzani wake Rais wa zamani wa Zimbabwe Robert Mugabe.
Morgan Tsvangirai alianzisha chama cha Movement for Democratic Change -MDC- mwaka 2000, na kuanza kutoa changamoto kwa Rais wa zamani wa nchi hiyo aliyekaa madarakani muda mrefu.
Kufuatia kifo hicho Bwana Tsvangirai, MDC inaelekea kugawanyika juu ya nani atakayeongoza uchaguzi hapo baadaye mwaka huu dhidi ya chama tawala cha Zanu PF, ambacho kwa sasa kinaongozwa na Emmerson Mnangagwa.