Msanii wa Bongo Fleva, Harmonize amevunja mkataba rasmi kimaandishi na waliokuwa wasanii wake Killy na Cheed.
Hatua hiyo imefikiwa katika ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) na kuthibitishwa na Katibu wake, Dk Kedmom Mapana.
Harmonize alitangaza kuvunja mkataba na wasanii hao kwa kuweka tangazo kwenye ukurasa wa lebo yake ya Konde Music Worldwide na hakuwa wazi kueleza sababu ya kufanya hivyo.
Kutokana na hatua hiyo Killy na Cheed walikimbilia Basata kufikisha malalamiko yao ya kutofuatwa kwa utaratibu wa kuvunjwa kwa mkataba huo ikiwemo kutopewa barua rasmi.
Vikao vya kuzikutanisha pande hizo mbili vilifanywa zaidi ya mara nne huku upande wa Harmonize akiwakilishwa na mwanasheria wake Musa Nassoro.
Hata hivyo mkataba wa kimaandishi wa kuachana uliwasilishwa na mwanasheria huyo ambapo wasanii hao waliridhia kuachana na lebo hiyo.
Meneja wa kina Cheed, Saty Sembe amesema kikubwa walichokuwa wanakipigania ni kupewa barua ya kimaandishi ili kuwa huru kufanya kazi zao ikiwemo kuweza kuingia mikataba na watu wengine.
Jambo la pili Sembe amesema walilokuwa wanalipigania ni kuachiwa kwa kurasa za mitandao yao ya kijamii ambayo ni moja ya chanzo cha kuwaingizia hela kwa kuuza kazi zao.
Wakati kuhusu Sh10 milioni kila mmoja anayotakiwa kulipwa msanii, Meneja huyo amesema watalipwa hata baadaye.
Cheed na Killy waliojiunga rasmi na lebo hiyo ya Konde Septemba 2020 wakitokea lebo ya King’s Music inayomilikiwa na msanii Ali Kiba.