Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete amewapoza wahitimu wa fani ya ualimu akisema wasikatishwe tamaa na tatizo la ajira katika sekta hiyo kwa kuwa ni suala la muda litakalokwisha muda mfupi ujao.
Dk Kikwete aliyasema hayo jana alipokuwa akiwajibu wahitimu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa waliopaza sauti wakimtaka amuombe Rais John Magufuli afungue milango ya ajira katika sekta hiyo na sekta nyingine za umma.
Kikwete amewaambia wahitimu 952 aliowatunuku vyeti vyao katika fani nne za Shahada za Elimu kwamba tatizo la uchelewaji wa ajira kwao litakwisha baada ya muda mfupi kwa kuzingatia kwamba Taifa lina mahitaji makubwa ya walimu.
Kikwete aliyetumia dakika zisizozidi tatu kuzungumza na wahitimu hao wakati akifunga mahafali hayo, alisema ataufikisha ujumbe huo kunakohusika kama alivyoombwa.
Akizungumzia maendeleo ya chuo hicho Mkuu wa chuo hicho, Profesa Bernadeta Killian amesema uongozi wa chuo unaendelea na mikakati mbalimbali ya kukiboresha ili kiendelee kuwa taasisi na mahali bora pa kutolea elimu, huduma za jamii kama vile ushauri na kuongeza udahili wa wanafunzi.
Amesema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006, chuo kimezalisha wahitimu 5,018 kama walimu katika fani mbalimbali.
Pamoja na mafanikio hayo na mengine mengi, Profesa Killian alisema chuo kinaendelea kuikumbusha serikali kuwa ruzuku inayotolewa kwa ajili ya uendeshaji na utekelezaji wa mipango mbalimbali bado ni ndogo na imekuwa ikishuka mwaka hadi mwaka.