Shirika lisilo la Kiserikali la Speak Up for Africa limemtunuku tuzo, rais mstaafu, Jakaya Kikwete, kutokana na uongozi wake wa kisiasa na utetezi wake kwa makundi ya jamii yaliyo katika mazingira magumu hususani wanawake na watoto.
Utoaji wa tuzo hiyo ya uongozi wa kisiasa na utetezi , umekwenda sambamba na hafla ya miaka mitano ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Speak up Africa.
Hafla hiyo iliyofanyika jana Alhamisi Jijini New York ilikuwa pia ni sehemu ya kuhamasisha uchangiaji wa shughuli za taasisi hiyo.
Mchango ambao umetambuliwa na Speak Up Africa, taasisi ambayo imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na Kikwete, ni katika maeneo ya upelekaji na usambazaji wa huduma za msingi za afya hususani afya ya mama na mtoto, udhibiti wa ugonjwa wa malaria kupitia kampeni ya Malaria Haikubaliki, usambazaji wa vyandarua vyenye viatilifu, kampeni ya lishe bora, na kampeni ya chanjo kwa watoto.
Pamoja na kutambua juhudi zake katika kuyasemea maeneo hayo, taasisi hiyo kupitia Mkurugenzi wake Mtendaji Bi. Kate Campana pia imemtambua kama kiongozi ambaye amekuwa mstari wa mbele wa kulisemea Bara la Afrika kila mara alipopata fursa ya kufanya hivyo wakati akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu.
Kikwete ameelezwa katika hafla hiyo iliyowashirikisha wadau wa kada mbalimbali, kama kiongozi wa kisiasa ambaye amezigusa nyoyo za watu wengi kujitolea kwa ajili ya watu wenye mahitaji ya kupata huduma za msingi za kijamii ambazo au wameshindwa kuzipata kutokana na kipato kidogo au haziwafikii kabisa.
Akipokea tuzo hiyo, amesema tuzo hiyo ni ya watoto wote Waafrika ambao ndiyo waliomfanya asimame mbele ya wageni waalikwa.
Amesema anamini katika ushirikiano na wadau mbalimbali kama akina Ray Chambers kupitia kampeni ya Hakuna Tena Malaria, Taasisi ya Billy na Melinda Gates na Gavi Vaccination Alliance ambayo anashirikiana nayo kwa karibu katika kampeni ya chanjo kwa wote.
Kikwete amewahakikishia watendaji wa Speak Up Africa kwamba ataendelea kufanya kazi nao kwa karibu kutokana kile alichosema amejionea mwenye kazi nzuri wanayoifanya.
Wengine waliopewa tuzo kwa kutambua michango yao kwa jamii ni pamoja na Professa Awa Marie Coll- Seck, Waziri wa Afya wa Senegal, Bibi Toyin Saraki, mwanzilishi wa Taasisi ya Wellbeing Afrika ambayo pia imekuwa ikitoa elimu na misaada kwa wanawake na watoto pamoja na elimu kwa wakunga na kutambua kazi nzuri, kubwa na ngumu ya kuwahudumia wanawake wenzao wanapojifungua. Pia alikuwemo Kabirou Mbodje ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wari.
Taasisi ya Speak Up Africa imeanzishwa na wanawake na inaongozwa na wanawake. Ni taasisi ambayo imejijengea uwezo na sifa kubwa ndani ya kipindi cha miaka mitano tangu kuanzishwa kwake.