Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla amesema Serikali kupitia Wizara yake inakusudia kuandaa mkakati maalum wa kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania nchini China ili kuongeza idadi ya watalii na mapato ya Serikali.
Dk. Kigwangalla amesema hayo ofisini kwake mjini Dodoma kwenye mazungumzo na Balozi wa China nchini, Mhe. Wang Ke ambaye alimtembelea kwa ajili ya kujitambulisha na kujadili uhusiano baina ya nchi hizo mbili katika sekta ya Uhifadhi na Utalii.
Amesema kuwa “Moja ya mkakati wangu kama Waziri mpya wa Wizara hii kukuza utalii ni kuweka mkakati wa kuleta watalii wengi kutoka China, China ni Taifa Kubwa lenye watu wengi, tunalenga zaidi kuwafikia watu wanaoishi maisha ya kati ambao ndio wanaopenda kutumia fedha zao kufurahia maisha”.
Waziri Kigwangalla amemuomba Balozi huyo kushirikiana na Serikali ya Tanzania kwa njia ya ushauri wa kitaalamu au wa kifedha kwa ajili ya kuandaa mkakati mahususi wa kulifikia soko la utalii la China.
Miongoni mwa mikakati waliojadiliana ni uwezekano wa kutumia fursa ya uwepo wa wawakilishi wa Televisheni ya CCTV ya China nchini Tanzania ambao wanaweza kutumika kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini na baadaye kuvitangaza nchini China na Duniani kote.