Mwanamuziki wa taarab nchini, Khadija Kopa amekiri kuwa hadi sasa amewahi kuwa kwenye ndoa nne tofauti.

Bi Khadija anasema kuwa, kuna kipindi aliomba talaka yake ya kwanza baada ya mume wake kumuacha akiwa mjamzito na kupotea kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili.

Anasema kuwa, wakati mume wake wa kwanza anarudi tayari alikuwa ameposwa na mume wa pili.

Khadija Kopa amesema kuwa, mume wake wa pili alikuwa mwenye vurugu na alikuwa na mazoea ya kulala nje mara kwa mara.

Anadai kwamba aliamua kujiondoa kwenye ndoa hiyo kwa kuhofia maisha yake huku akisema kuwa wakati mumewe aliwahi kumburuza chini akiwa mjamzito.

Bi Khadija anasema kuwa, baada ya kuondoka kwenye ndoa ya pili aliolewa na mwanaume tapeli ambaye hakuwapenda watoto wake.

Anasema watoto wake wakiongozwa na marehemu Omari Kopa walimshinikiza aachane na ndoa hiyo baada ya mumewe kukamatiana visu na kifungua mimba wake huyo.

Mkongwe huyo wa muziki yapata miaka 30 sasa, anasema kuwa, wakati anaomba mumewe huyo wa tatu talaka, aliiandika haraka ila akaanza kujuta siku tatu baadaye.

Bi Khadija anasema kwamba mume wake wa mwisho, Jaffari Ally ambaye alifariki dunia takriban miaka tisa iliyopita ndiye aliyekuwa mzuri kati ya wote.

Anasema marehemu Ally aliwapenda watoto wake na vilevile wanawe walimpenda pia.

Bi Khadija amewahi kuolewa na mume mwenye wake watatu tayari na kueleza kwamba hakuwahi kuzozana na wake wenzake.

Kwa sasa hana hamu ya ndoa kwa kuwa anahofia kukutana na mwanaume ambaye hataridhia kuwa naye. Hata hivyo, anasema wapo wanaume wengi ambao wamekuwa wakimmezea mate wakitamani kumuoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *