Kesi inayomkabili Mbunge wa Geita , Joseph Kasheku Msukuma na madiwani nane imesogezwa mbele baada ya upande wa mashitaka kudai upelelezi haujakamilika.
Kesi hiyo ambayo ilikuwa isikilizwe jana imepangwa kutajwa tarehe 10 mwezi wa 11 mwaka huu ambapo washitakiwa wote wapo nje kwa dhamana.
Kwa upande wake wakili anayewatetea washitakiwa Bw Deo Mgengeli alielezea hatua ambayo imeendelea siku ya jana mahakamani hapo kuwa shauri limekuja na kwamba limetajwa na hadi sasa hakuna mshitakiwa ambaye ameongezeka hivyo mahakama imeamua tarehe Kumi mwezi wa 11 wawasili mahakamani kusikiliza tena kesi hiyo.
Aidha wakili Mgengeli alizungumzia suala la madiwani wengine waliokamatwa na jeshi la polisi na kutofikishwa mahakamani akasema kuwa kukamatwa kwa madiwani hao ni jambo la kawaida kwani ni swala la upepelezi kwa makosa ya jinai na kwamba alhamisi wanatakiwa kwenda tena polisi ili kujua ni kipi ambacho kinaendelea ila hadi sasa hawana kosa lolote.
Awali washitakiwa hao kwa pamoja walifikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita Septemba 19 mwaka huu.
Washitakiwa wanakabiliwa na mashitaka ya kufanya mkutano bila kibali, kuziba barabara na uharibifu wa bomba la maji linaloelekea kwenye mgodi wa dhahabu wa GGM.