Kesi iliyokuwa inamkabili mke wa bilionea Erasto Msuya, anayeitwa Miriam Msuya imefutwa leo Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mahakama hiyo imemwachia huru Miriam Msuya na mwenzake baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kugoma kuifanyia mabadiliko hati ya mashtaka pamoja na kupewa siku tatu za kufanya hivyo.
Hakimu Mwambapa aliamua kuwaachia huru Miriam na Revocatus Muyela wanaoshtakiwa kumuua kwa kukusudia dada wa bilionea huyo, Aneth Msuya Mei mwaka jana maeneo ya Kibada Kigamboni, jijini Dar es Salaam.
Hakimu Godfrey Mwambapa ameifuta kesi hiyo baada ya upande wa jamhuri kushindwa kuifanyia marekebisho hati ya mashataka ambayo ilibainika kuwa ni mbovu.
Wakili wa serikali, Hellen Moshi alidai ofisi ya DPP haiwezi kubadilisha hati hiyo sababu iko sahihi kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Wakili wa utetezi, Peter Kibatala amedai jamhuri wamekaidi amri ya mahakama hivyo wateja wake waachiwe huru kwani hakuna hati ya mashtaka inayowashikilia.
Washtakiwa waliachiwa huru lakini walichukuliwa tena na polisi kuelekea kituoni.
Source: Mtanzania