Mahakama Kuu Kanda ya Tanga imetupilia mbali rufaa ya kusikiliza upya shauri la mirathi ya marehemu Mohammed Shosi lililofunguliwa na Swabaha Mohamed Ali.
Mwanzoni mwa mwezi huu, Swabaha aliyedai kuwa ni mke wa marehemu Shosi, aliibuka mbele ya Rais Dk. John Magufuli wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria na kulalamika kutaka kudhulumiwa haki yake ya mirathi.
Rufaa hiyo uamuzi wake ulitakiwa kutolewa kesho, lakini hata hivyo ulitolewa juzi na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Amour Hamis.
Katika kesi hiyo ambayo Swabaha aliifungua dhidi ya Saburia Shosi, ambaye ni mtoto wa marehemu Shosi aliyeteuliwa kuwa msimamizi wa mirathi ya marehemu baba yake, Jaji Amour akitoa uamuzi alisema mahakama hiyo imeridhika na hukumu iliyokuwa imetolewa hapo awali na mahakama ya wilaya pamoja na ile ya mwanzo.
Katika hilo, jaji huyo aliamuru taratibu nyingine za uendeshaji wa mirathi kuendelea kama ilivyokuwa imeamuliwa na mahakama ya mwanzo na ile ya wilaya.
Katika kesi iliyofunguliwa na Saburia katika Mahakama ya Mwanzo Desemba 16, 2012, kuomba awe msimamizi wa mirathi, mahakama hiyo ilimruhusu.
Hata hivyo, mwaka 2015 Swabaha alikata rufaa Mahakama ya Wilaya akifungua kesi ya kuzuia mali za marehemu, ambayo nayo upande wa akina Saburia walishinda huku mahakama ikimuamuru aendelee kuwa msimamizi wa mirathi.
Katika umuzi wake wa sasa, Jaji Amour alisema kuwa pamoja na hukumu hiyo, Swabaha ambaye alikuwa akiwakilishwa na wakili wake Ngomela, atatakiwa kumlipa Saburia gharama zote za uendeshaji wa kesi hiyo.