Kesi ya kutoa lugha chafu inayomkabili Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima inatarajiwa kuendelea kusikilizwa Oktoba 27, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba amesema leo baada ya Wakili wa Serikali Jacqueline Nyantori kudai kuwa wameondoa kusudio la kukata rufaa.

Kesi hiyo ilisimama kwa zaidi ya miezi minne baada ya upande wa Jamhuri kuwasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi wa mahakama kukataa kupokea CD iliyotolewa kama sehemu ya ushahidi wa upande wa Jamhuri.

Mahakama ilikataa kupokea kielelezo hicho kwa kuwa hakijakidhi vigezo na wameshindwa kukielezea ipasavyo kwa kukitolea maelezo ya kutosha lakini upande wa Jamhuri uliwasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga uamuzi huo katika Mahakama Kuu.

Hakimu Simba amesema kesi hiyo imeshasimama kwa miezi minne, haijasikilizwa hivyo aliwataka upande wa Jamhuri, kueleza kama wana nia ya kuondoa rufaa hiyo ili kuruhusu kesi kuendelea kusikilizwa.

Wakili Nyantori amesema wana nia hiyo ili kuruhusu kesi hiyo kuendelea kusikilizwa.

Katika kesi hiyo, Gwajima anadaiwa kati ya Machi 16 na 25, 2015 eneo la Tanganyika Packers Kawe alitumia lugha chafu na kumdhihaki Askofu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.

Inadaiwa Gwajima alimdhihaki Pengo kwa kusema, ni mpuuzi mmoja, mjinga mmoja, asiyefaa mmoja, anaitwa Askofu Pengo, aliropoka sijui amekula nini, mimi naitwa Gwajima namwita mpuuzi yule, mjinga yule na kuonesha Pengo ni mtoto mwenye akili ndogo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *