Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa imemaliza maelekezo waliyopewa na Mkurugenzi wa Mashtaka DPP katika jalada la kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva na mwenzake.
Hayo yameelezwa na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Leonard Swai, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Victoria Nongwa wakati kesi hiyo ilipoitishwa kwa ajili ya kutajwa.
Swai alidai, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika ila kwa upande wao washamaliza maelekezo waliyopewa na DDP kuhusu kukamilisha upelelezi katika baadhi ya maeneo ambapo tayari wamerudisha jalada la kesi hiyo ili aweze kulipitia tena.
Pia Swai amedai kuwa mshtakiwa Aveva ameshindwa kufikia mahakamani kwa sababu anaumwa, pia amepelekwa Kliniki.
Baada ya kueleza hayo, Hakimu Nongwa aliahirisha kesi hiyo hadi March 1,2018 kwa ajili ya kutajwa.
Katika kesi hiyo, mshtakiwa mwingine ni Godfrey Nyange ambapo kwa pamoja wanadaiwa kula njama ya kughushi fomu ya maombi ya kuhamisha fedha ya March 15, 2016 wakionesha Klabu ya Simba inalipa mkopo wa USD 300,000 kwa Evans Aveva wakati si kweli.
Kuhusu shtaka la kutakatisha fedha, Aveva anadaiwa kuwa kati ya March 15, 2016 katika benki ya Baclays Mikocheni alijipatia USD 300,000 wakati akijua zimetokana na kughushi.