Rais Uhuru Kenyatta anaongoza matokeo ya uchaguzi yanayoendelea kutangazwa nchini Kenya baada ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu nchini humo jana.

Katika matokeo yaliyokuwa yametangazwa kufikia saa tatu asubuhi leo, Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee alikuwa akiongoza akiwa na kura 7,461,933 (54.64%) akifuatwa na Raila Odinga wa muungano wa upinzani National Super Alliance (Nasa) aliyekuwa na kura 6,079,136 (44.51%). Matokeo hayo ni ya vituo 36659 kati ya 40,883.

Muungano wa Nasa umepinga matokeo yanayoendelea kutangazwa na tume hiyo na kusema si sahihi kulingana na matokeo hayo.

Odinga amesema IEBC imefanya makosa kwa kutangaza matokeo hayo bila kuwaonyesha maajenti wa vyama Fomu 34A, kubainisha matokeo hayo yametoka katika vituo gani.

Katika baadhi ya vituo, shughuli ya upigaji kura ilichelewa kuanza na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (IEBC) iliongeza muda kufikia wakati uliokuwa umepotezwa kabla ya kufungua vituo.

Kisheria, vituo vilitakiwa kufunguliwa saa kumi na mbili asubuhi na kufungwa saa kumi na moja jioni saa za Afrika Mashariki.

Lakini katika baadhi ya maeneo, mvua kubwa ilitatiza uchukuzi na upigaji kura na kwingine hitilafu za kimitambo zikachangia kukwamisha upigaji kura. Muda wa kufungwa kwa vituo uliongezwa kwa vituo vilivyochelewa kufunguliwa.

Wengi wanahofia uwezekano wa kutokea tena kwa ghasia za baada ya uchaguzi sawa na ilivyotokewa baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ambapo watu zaidi ya 1,100 walifariki na wengine 600,000 kuachwa bila makao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *