Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amepinga kufanyika kwa mazungumzo yoyote na kiongozi wa upinzani Raila Odinga kumaliza mgogoro wa kisiasa nchini Kenya uliosababishwa na uchaguzi mkuu uliokwisha.
Katika hotuba yake muda mfupi baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa marudio , rais Kenyatta amesema kuwa mpinzani wake mkuu Raila Odinga atakwenda mahakamani kwa mara nyengine tena kupinga uchaguzi wake.
Kenyatta amewataka wapinzani wake wa Nasa kutumia njia zote za kisheria katika kupigania haki yao.
Wawacheni mwanzo watumie njia zote za kisheria zilizosalia wawacheni wafanye wanachotaka.
Rais Kenyatta pia alimshutumu Raila Odinga kwa kujiondoa katika uchaguzi huo uliofanyika Alhamis iliyopita.
Katika uchaguzi wa marudio Uhuru alijipatia kura 7,483,895 huku Raila Odinga akijipatia kura 73,228 hata baada ya kujiondoa katika uchaguzi huo.