Serikali ya Kenya imetangaza kuwa siku ya kesho itakuwa ya mapumziko ili kuwapa wananchi muda wa kutosha kwa maandalizi ya uchaguzi wa marudio unaotarajiwa kufanyika Alhamisi ya Oktoba 26.
Kaimu Waziri wa Mambo ya Ndani Fred Matiang’i ameweka notisi hiyo leo katika Gazeti la Serikali na kufahamisha kwamba Alhamisi ya Oktoba 26 itakuwa siku ya mapumziko pia.
Wakenya watakwenda kwenye vituo kuchagua kati ya Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi Mkuu wa muungano wa upinzani (Nasa) Raila Odinga ingawa alitangaza kujitoa kwenye uchaguzi huo wa marudio siku chache zilizopita.
Hata hivyo Raila amewataka wafuasi wake kususia uchaguzi huo na kampeni zake kubwa kwa sasa ni kuhakikisha haufanyiki kwa madai Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imeshindwa kutekeleza marekebisho muhimu ambayo amekuwa akitaka yafanyike tangu yalipobatilishwa matokeo ya uchaguzi wa Agosti 8.