Shirika la ndege la Kenya, Kenya Airways limezindua uuzaji wa tiketi za safari ya kwanza kabisa ya ndege zake za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi Marekani.
Shirika hilo linapanga kufanya safari yake ya kwanza mnamo 28 Oktoba, hatua itakayoifanya Kenya Airways kuwa shirika la kwanza kutoka Afrika Mashariki kuwa na safari za moja kwa moja Marekani.
Ndege za shirika hilo litakuwa zinafasiri moja kwa moja hadi uwanja wa ndege wa JFK, New York.
Meneja Mkurugenzi wa Kenya Airways Sebastian Mikosz akizungumza wakati wa uzinduzi huo amesema safari hizo zitawafaa sana katika mpango wake wa ukuaji.
Kenya Airways itafanikisha safari hizo kwa ushirikiano na shirika la Delta Airlines la Marekani.
Kwa mujibu wa Bodi ya Utalii Kenya, Kenya hupokea watalii 100,000 kutoka Marekani kila mwaka na safari hizo zinatarajiwa kuifanya nafuu kuzuru Kenya kwa kupunguza muda wa kusafiri na gharama.
Kuzinduliwa kwa safari hizo ni matunda ya mashauriano ya muda mrefu kati ya Kenya na serikali ya Marekani.
Kenya ilipewa masharti ya kuimarisha usalama, ikiwa ni pamoja na kuwatenganisha abiria wanaotua na wanaoondoka, kufanya salama njia za safari ya ndege na pia kuweka ua katika uwanja wa ndege wa JKIA.
Kenya ilipewa hadi ya Kiwango cha Kwanza kutoka kwa Shirika la Safari za Ndege la Marekani Februari mwaka jana na kuifungulia njia Kenya Airways kufanya safari za moja kwa moja.