Shirika la Ndege za Kenya (Kenya Airways) limepewa kibali cha usalama na maafisa wa Marekani kuanza safari za ndege za moja kwa moja hadi Marekani.
Waziri wa Uchukuzi wa Kenya, James Macharia amesema kibali hicho kimetokana na kuimarishwa kwa miundombinu katika uwanja mkuu wa ndege mjini Nairobi.
Macharia alisema Kenya inatumai kuwa hatua hiyo itaimarisha biashara kati yake na Marekani na kuongeza mgawo wake wa watalii wa Marekani wanaotembelea nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Serikali ina hisa katika shirika la ndege la Kenya Airways na hivi karibuni ilimaliza kujenga kituo kipya cha abiria katika uwanja huo na inapanga kutumia fedha zaidi katika kuuboresha Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta.