Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dotto James ameshindwa kuhudhuria kikao cha kamati ya kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC)  na kusababisha kushindwa kupitia hesabu za Mfuko wa Pensheni wa PSPF.

Katibu Mkuu huyo ndiye alipaswa kwenda mbele ya kamati hiyo na viongozi wa mfuko huo kwa kuwa PSPF haina bodi na kwa mujibu wa Kanuni za Bunge, zinataka shirika ambalo halina bodi, Katibu Mkuu anayewakilisha serikali kufika mbele yake.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Naghenjwa Kaboyoka amesema kamati imesikitishwa na kitendo cha Katibu Mkuu huyo na kubainisha kuwa wajumbe, wamekitafsiri kama ni dharau kwa kamati hiyo na Bunge.

Amesema hali ya mfuko huo hairidhishi kwani dalili zinaonesha kuwa, unakaribia kufa kutokana na kuelemewa na madeni ambayo mengi kati yake unaidai serikali.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Aeshi Hilaly amesema mahudhurio ya katibu huyo katika kamati hiyo ni muhimu kwani anapaswa kujibu namna serikali itakavyouokoa mfuko huo kutokana na kuendelea kuwa katika hali mbaya ya kifedha.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *