Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Pombe Magufuli ametengua uteuzi wa katibu mkuu wa wizara ya Nishati na Madini Prof. Justin Ntalikwa.

Rais Magufuli amefanya hivyo siku chache baada ya kufanya ziara ya kushtukiza bandari ya Dar es Salaam lakini haijabainika iwapo kuna uhusiano kati ya ziara hiyo na kutenguliwa kwa Ntalikwa.

Rais Magufuli alifanya ziara hiyo kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa nyakati tofauti, juu ya kudhibiti udanganyifu wa mizigo inayoingia na kutoka nchini kupitia bandari hiyo, ikiwemo usafirishaji wa mchanga wa madini kwenda nje ya nchi.

Katika ziara hiyo Rais Magufuli alishuhudia makontena 20 ya mchanga wenye madini kutoka kwenye migodi iliyopo kanda ya ziwa, ambayo yamezuiliwa kusafirishwa nje ya nchi tangu alipotoa agizo la kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga nje ya nchi tarehe 2 Machi, 2017.

Pamoja na kushuhudia makontena hayo, Rais Magufuli alimuagiza mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP – Ernest Mangu na vyombo vingine vya dola, kuhakikisha mchanga wa madini unashikiliwa popote ulipo, mpaka hapo uchunguzi wa kina utakapofanyika kubaini ukweli.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *