Aliyekuwa mshindi wa tuzo la Miss World Kenya 2016 , Roshanara Ebrahim, amepokonywa taji hilo baada ya kukumbwa na sakata.

Kulingana na gazeti la The Standard nchini Kenya, Roshanara mwenye umri wa miaka 23, alishinda taji la mwaka uliopita na alikuwa anatarajiwa kuiwakilisha Kenya kwenye mashindano ya Miss World, mwishoni mwa mwaka huu.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, wasimamizi wa Miss World Kenya, kampuni ya bidhaa za urembo, Ashleys imeandika kama ifuatavyo ‘Kuanzia sasa, Roshanara hatoiwakilisha Kenya nchini na hata kimataifa kama Miss World. Tumefahamishwa kuhusu sakata kubwa inayomkumba Roshanara Ebrahim, ambayo inakiuka sheria na masharti ya Miss World Kenya.

Tunatekeleza sheria zetu na tunatarajia wanamitindo wetu kusimamia maisha yao ya kibinafsi.

Kulingana na gazeti hilo , Roshanara ameandika kukubaliana na uamuzi huo na kuwasihi warembo wenye umri mdogo kuhakikisha maisha yao ya kibinafsi, hayaathiri jukumu lao la Miss World.

Kabla ya uamuzi wa ofisi ya Miss World Kenya, Roshanara alilazimika kujitetea dhidi ya madai yaliomhusisha kuwa na uhusiano na mwanasiasa mashuhuri.

Tayari ofisi ya Miss World Kenya, imeahidi kumtangaza mwanamitindo atakayejaza pengo lililoachwa na Roshanara Ebrahim siku chache zijaazo.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *