Beki wa Simba, Shomari Kapombe ameibuka na kujibu tuhuma alizotupiwa na bosi wake, Zacharia Hans Poppe.
Hans Poppe alimshushia lawama beki huyo kuwa amepona majeraha yake yanayomkabili na anakaa nje kwa uoga wake huku akiendelea kula mshahara wa bure wa kila mwezi tangu asajiliwe na Simba.
Kapombe tangu amejiunga na Simba msimu huu wa Ligi Kuu Bara kwa dau la shilingi milioni 35, hajacheza mechi yoyote kutokana na majeraha aliyoyapata akiwa na Timu ya Taifa.
Mchezaji huyo amesema yeye bado mgonjwa na haogopi kucheza kama anavyoeleza Hans Poppe kwani hakuna kipya kitakachomuogopesha.
Kapombe amesema, kwa mujibu wa daktari wake, atarejea uwanjani kucheza mechi za ligi kuu kwenye mzunguko wa pili akiwa fiti kabisa.
Aliongeza kuwa, kuhusiana na kuvunja mkataba wake, yeye hana tatizo kikubwa ni kufuata taratibu za kuuvunja.