Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel amezindua jumba jipya makao makuu ya Umoja wa Afrika ambalo limepewa jina la rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Kambarage Nyerere.
Jumba hilo ambalo jina lake kamili ni Jumba la Amani na Usalama la Julius Nyerere limejengwa kwa ufadhili kutoka Ujerumani.
Litakuwa makao ya idara ya Amani na Usalama ya AU na litatumiwa pia na maafisa wa kutoa tahadhari ya mapema kuhusu mizozo barani pamoja na kuratibu juhudi za kulinda amani za AU.
Ujenzi wa jumba hilo, ambalo ukubwa wake wa sakafu ni mita 13,500 mraba na linaweza kutumiwa na wafanyakazi 360, uligharimu euro 27 milioni.
Jumba hilo lina ofisi za kufanyia kazi, vyumba vya mikutano vya kutumiwa na Baraza la Amani na Usalama, chumba cha kuratibia shughuli, maktaba na vyumba vya shughuli za pembeni.
Mwalimu Nyerere, ambaye alikuwa rais wa Tanzania hadi 1985, alikuwa mmoja wa viongozi waanzilishi wa Muungano wa Nchi za Afrika (OAU) ambao sasa ni Umoja wa Afrika (AU).