Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki ameitaka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kuhakikisha wanasajili mtumishi yeyote hata kama hana vyeti na ndani ya siku 14 mhusika huyo anatakiwa arejeshe vyeti vyake kwa Ofisa Utumishi.

Kairuki pia ameipongeza Nida kwa juhudi za kuendelea kusajili watumishi wa umma katika kuhakikisha wanapata vitambulisho vya taifa.

Amesema kila mtumishi wa umma anatakiwa kuhakikisha kuwa anapata Kitambulisho cha Taifa kabla ya Desemba mwaka huu na kuwashukuru wale wote waliojitokeza mpaka sasa kwa ajili ya suala hilo.

Kwa upande wake mkurugenzi wa Wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, Eliud Leonard aliiomba serikali kuongeza muda wa usajili wa vitambulisho hivyo kutokana na kuwa mdogo huku wilaya hiyo ikiwa na watumishi wengi na mashine hizo zimekuwa zikisajili watu 150 katika vituo vya Misungwi na Usagara.

Eliud amesema wilaya yake ina vitongoji 723, vijiji 113, kata 27 na tarafa nne, hivyo imekuwa vigumu kufika sehemu za vijijini kutokana na uhaba wa usafiri.

Amesema wilayani hapo hadi sasa kuna walimu wa elimu ya msingi 511 huku 37 wakiwa hawajahakikiwa na walimu 37 wana vyeti vyenye utata. Watumishi wa Afya waliohakikiwa ni 525 ambapo watumishi 15 hawajahakikiwa na watumishi 66 wana vyeti feki.

Ofisa Msajili katika mkoa huo, Daudi Hashim alisema usajili wa vitambulisho vya Taifa kwa watumishi wa umma unaendelea na mpaka sasa wamesajili 10,634 wakiwamo walimu.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *