Makamu mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange maarufu kama Kaburu ameipongeza Yanga kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Simba imeshindwa kumaliza vizuri ligi ya msimu huu, baada ya kuongoza kwa tofauti ya pointi nane kwa muda mrefu hadi ilipokuja kuenguliwa kileleni kufuatia kipigo cha mabao 2-1, kutoka kwa Kagera Sugar.
Kaburu alisema wanajisikia vibaya kuukosa ubingwa wa msimu huu, lakini hawana budi kuwapongeza Yanga kutokana na kufanikiwa kutetea taji hilo kwa bahati dakika za mwisho.
Kiongozi huyo alisema baada ya kupoteza taji hilo nguvu zao kwa sasa wamezielekeza kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la FA, dhidi ya Mbao FC utakaopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri Dodoma Mei 28 mwaka huu.
Kaburu alisema wamepanga timu yao kuipeleka Zanzibar kupiga kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo huo wa fainali lengo ni kuhakikisha wanashinda ili kushiriki na michuano ya kimataifa
Baada ya mchezo wao wa mwisho wa ligi dhidi ya Mwadui keshokutwa, kikosi chao kitaondoka Dar es Salaam Jumapili kwa ajili ya kambi hiyo ambayo wanaamini itakuwa na mafanikio kutokana na ari waliyokuwa nayo wachezaji na viongozi.