Jumla ya Watanzania wanaorudishwa nchini kutokea nchi ya Msumbiji imeendelea kuongezeka hadi kufikia watu 193 hadi sasa.
Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Mtwara, Naibu Kamishina wa Uhamiaji, Rose Mhagama, zimesema kuwa hadi jana kulikuwa na Watanzania 193 waliopokelewa kutoka Msumbiji kwa kupitia katika Kijiji cha Kilambo wilayani Mtwara.
Mhagama amesema kundi la kwanza la watu 58 lilipokelewa siku tatu zilizopita, likafuatiwa na kundi la Watanzania wengine 122 waliopokewa juzi na jana walipokelewa 13 na hivyo kufanya idadi hiyo kufikia 193 waliofukuzwa nchi hiyo jirani yenye uhusiano wa kindugu na Tanzania.
Amesema ofisi yake hivi sasa inahakiki utanzania wao na baadaye kuwasaidia kuwarudisha kwao kulingana na taarifa watakazopata na kuzihakiki kwa kuwa licha ya kudai kuporwa hati zao za kusafiria, wapo baadhi wanaokumbuka namba na hivyo wanaziingiza katika mfumo ili kuzitambua.
Kwa mujibu wa Watanzania hao waliosombwa na msako huo, wanadai kuwa kinachofanyika huko ni unyanyasaji na uporaji wa mali na fedha za wageni unaondeshwa na polisi kwa kisingizio cha wahamiaji haramu.
Wamedai kuwa katika msako huo wakibaini ni Mtanzania, unapororwa kila kitu simu fedha gari na kuchukuliwa mikono mitupu na watoto wako na kutupwa mahabusu hadi siku ya kupelekwa nchini kwao.