Mapigano yamezuka tena upya baina ya pande hasimu nchini sudan kusini ambapo vikosi vya serikali vinapambana dhidi ya vikosi vya aliyekuwa makamo wa rais nchini humo.
Kuna hofu kuwa Sudan kusini huenda ikatumbukia tena kwenye vita vya kiraia.
Walioshuhudia wamesema wamesikia milio ya risasi katika mji muhimu wa Yei, kusini magharibi mwa Juba, kwenye barabara inayounganisha Juba na taifa jirani la Uganda.
Vikosi vitiifu kwa naibu rais, Riek Machar, vimesema kwamba vikosi vya serikali viliwashambulia katika maeneo yao siku ya jumamosi.
Mwezi uliopita vikosi vitiifu kwa rais Salva Kiir na Riek Machar vilikabiliana mjini Juba, katika makabiliano yaliyoifanya UN kutuma walinda 400 zaidi nchini humo.
Hata hivyo Bw Kiir amesema hataruhusu Umoja wa Mataifa kuchukua udhibiti wa nchi yake na hatashirikiana tena na umoja huo.
Uhasama wa kisiasa baina bwana Kiir na bwana Machar uliishia kuwa mapigano mwaka 2013.
Wawili hao walitia saini mkataba wa amani mwaka 2015 japo mapigano ya mara kwa mara yamekuwa yakiendelea baina ya pande hasimu.