Msanii wa vichekesho, Joti amefunguka na kusema kuwa ana uhakika atashinda tuzo kwenye tuzo za Zikomo Afrika zitakazofanyika mwaka huu.
Joti ameyazungumza hayo katika mkutano ulioandaliwa na Bodi ya filamu kwa ajili ya kuwapongeza wasanii walioteuliwa katika tuzo hizo.
Joti amesema katika kinyang’anyiro hicho anashindanishwa katika kipengele cha mchekeshaji bora nchi za Afrika Mashariki na Kusini na anaona hakuna mpinzani wake.
“Mpaka sasa najiona ni mshindi katika tuzo hizo, kikubwa watu waendelee kupiga kura ili nirudi na ushindi wa kishindo,” amesema Joti mwenye kipaji cha kuvaa uhusika wa babu,mtoto,kijana na mdada.
Emmanuel Ndumukwa, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Filamu kutoka bodi ya filamu alisema kitendo cha wasanii zaidi ya 23 wa filamu kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho ni wazi kuwa tasnia ya filamu nchini inakuwa na inafutiliwa na nchi mbalimbali.
Kutokana na hatua hiyo aliomba Watanzania kuwapigia kura wasanii hao kwa kuwa wakishinda ni nchi nzima itakuwa imeshinda na pia ni moja ya njia ya kukuza sanaa hiyo.
Akielezea hali ilivyo katika mchuano huo, alisema ushindani unaonekana mkubwa katika nchi ya Namibia, Afrika Kusini na Tanzania.
Tuzo hizo zinazotarajiwa kutolewa Oktoba 15, 2022 jijini Lusaka nchini Zambia zimelenga kutambua watu mbalimbali walio katika kazi za sanaa, masuaa ya haki za binadamu na ujasiriamali.