Mchekeshaji maarufu nchini, Lucas Mhavile ‘Joti’ aligonga vichwa vya habari mara baada ya kuwepo taarifa zilizodai kuwa nyumba yake iliyopo Kibada, Kigamboni imevunjwa ili kupisha upanuzi wa barabara, sasa Joti ameeleza kilichotokea.
Joti amesema si kweli kwamba nyumba yake imevunja bali ni ukuta ndio umewekwa alama ya X ila amekiri kuwepo kwa zoezi hilo.
Pia amesema ‘’Wanapanua barabara huku kwetu, lakini huo upanuzi wa barabara haujahusiana na ubomoaji wa nyumba, wengi wanajua nyumba yangu ndio inabomolewa lakini sivyo, kinachobomolewa ni ukuta tu,’’.
Kwa mujibu wa Afisa Manispaa ya Kigamboni, Davidi Langa wakazi zaidi ya 100 wa Kibada na Kisarawe wilayani Kigamboni nyumba zao zimewekea alama ya X na kutakiwa kubomolewa ili kupisha ujenzi wa barabara.
Chanzo cha tatizo ni Wizara ya Ardhi, Nyumba Maendeleo ya Makazi iliyopima maeneo hayo, Tanroad walikuwa bado hawajaweka alama zao za barabarani na viwanja hivyo ni vya muda mrefu, hivyo wamekuja kuweka wakati vimeshaendelezwa, hata hivyo Mkuu wa wilaya hiyo, Hashim Mgandilwa ameingilia kati suala hilo.