Mwanamuziki maarufu nchini Uganda, Jose Chameleone ametangaza rasmi kujiunga na masuala ya siasa kama alivyofanya msanii mwenzake, Bobi Wine.
Kutokana na kitendo hicho cha Chameleone kutangaza kujiiungiza kwenye siasa inaelekea umekuwa ni mtindo wa kawaida kwa wanamuziki maarufu kugeukia siasa baada ya kuwa na ushawishi mkubwa kwa wananchi.
Chameleone ambaye jina lake halisi ni Joseph Mayanja amesema kuwa anataka kuwa Meya wa mji mkuu wa Uganda Kampala hivyo ameamua kujiingiza kwenye siasa ili kuwa karibu zaidi na mashabiki wake ambao ni wananchi.
Moja ya nyimbo zake zinazofahamika ni ule wa Shida za Dunia, unaozungumzia matatizo yanayowakabili watu katika jamii tofauti nchini Uganda na Afrika kwa ujumla.
Akielezea matarajio yake, amesema:”Wakati huduma zinapokuwa katika hali mbaya, watu wanaanza kuamka .Watu wana kiu ya uongozi unaofaa na hawajaupata”.
Chameleone anaaminiwa kuwa amekuwa mfuasi wa chama tawala cha NRM, ambapo amekuwa akitumbuiza kwenye matukio ya chama hizo.
Chameleone hakuficha urafiki wake na mbunge wa Kyadondo mashariki Bobi Wine, hususan pale Wine alipojipata katika utata wa kisiasa na kukamatwa na maafisa wa polisi na kuwekwa mahabusu alimtembelea mahabusu kumfariji.