Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika harambee ya kukusanya fedha kiasi cha Sh. bilioni moja, kwa ajili ya ukarabati wa Shule ya Sekondari Lindi iliyoungua Julai 2016.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema harambee hiyo itafanyika kesho jijini Dar es Salaam.

Zambi amesema maandalizi yote kwa ajili ya harambee hiyo yamekamilika na inatarajia kuhudhuriwa na wadau wa sekta ya elimu nchini.

Amesema harambee hiyo imepanga kukusanya Sh. bilioni moja ikiwa ni karibu nusu ya mahitaji ya Sh. bilioni mbili zinazotakiwa kwa ajili ya ukarabati wa shule hiyo kongwe.

Mkuu wa mkoa huyo alikiri kuwa mkoa wake ni mmoja kati ya inayofanya vibaya kwenye matokeo ya mitihani ya kitaifa, lakini akasema hatua zimechukuliwa kurekebisha, ikiwamo kupima uwezo wa walimu.

Kwa upande wake, Ofisa Elimu wa Mkoa huo, Emmy Mchuchuri, alitaja changamoto zinazoukabili mkoa huo katika kutoa elimu kuwa ni miundombinu mibovu, uzembe wa walimu, utoro na kutokuwapo kwa chakula cha mchana shuleni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *